ARIMO YACHAPISHA ORODHA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA CHUO 2026/2027 (AWAMU YA KWANZA)

Imewekwa: 24, August 2026

Morogoro, Tanzania – Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kimeendelea kuthibitisha uongozi wake katika fani za upimaji ardhi, uandaaji ramani, upangaji miji na usimamizi wa ardhi kwa kuchapisha rasmi orodha ya wanafunzi wapya waliochaguliwa kujiunga na masomo kwa mwaka wa masomo wa 2026/2027 – Awamu ya Kwanza

Akizungumza na safu hii, Afisa Uandikishaji wa ARIMO Bw. Moses Maletelwa alithibitisha kuwa jumla ya wanafunzi 266 wamechaguliwa kujiunga na chuo hicho. Uandikishaji huu unahusu programu kuu nne ambazo ni: Geographical Information System (GIS), Geomatics, Land Management, Valuation and Registration (LMVR), pamoja na Urban and Regional Planning (URP).

Orodha kamili ya wanafunzi waliochaguliwa imechapishwa na inapatikana kupitia tovuti rasmi ya chuo kwa marejeo. Hatua hii inaleta uwazi na kuwapa waombaji fursa rahisi ya kuthibitisha nafasi zao za uandikishaji.

Katika taarifa tofauti, Mkuu wa Taaluma wa ARIMO Bw. Pius Kafefa aliwapongeza wanafunzi wote waliobahatika kuchaguliwa. Aidha, aliwahimiza kujiandaa kwa safari ya kitaaluma yenye mabadiliko makubwa, inayosisitiza maarifa, ubunifu na umahiri wa kitaaluma katika sekta ya ardhi na maendeleo ya miji.