ARIMO WAJA KIVINGINE

Posted On: 17, September 2018

ARIMO WAJA KIVINGINE

Chuo cha Ardhi Morogoro kina historia ndefu ya utoaji wa mafunzo katika fani ya upimaji ardhi na utengenezaji wa Ramani. Chuo hiki kilianza kama sehemu (Campus) ya iliyokuwa Taasisi ya Ardhi Dar es Salaam mwaka 1978 kabla ya kuwa chuo kinachojitegemea mwaka 1996. Ni takribani miaka arobaini sasa tangu kianzishwe.

Hivi karibuni ARIMO kimekamilisha maandalizi ya mtaala wa kozi ya Mipango Miji na kuiwakilisha katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa ajili ya kupata Ithibati. Habari ya kufurahisha ni kwamba, NACTE wameridhishwa na andiko la mtaala na kuliidhinisha. Hiyo ni kusema kuwa, kwa sasa kozi ya mipango miji itatolewa ARIMO.

Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro, Dkt Adam Nyaruhuma akiongea na safu hii hivi karibuni alisema ARIMO wamejiandaa kutoa mafunzo ya kozi hiyo ya Mipango Miji katika ubora ule ule ambao wamekuwa wakiutoa katika kozi ya upimaji ardhi. Ikumbukwe kuwa ARIMO wamekuwa na sifa nzuri ya kutoa wahitimu wanaofanya vizuri katika soko la upimji ardhi nchini kote Tanzania kwa miaka mingi sasa.

Naye Msajili wa wanafunzi Bw Musa H. Musa na Afisa Utumishi wa ARIMO Bi. Rebeca Kamihanda kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuanza kwa kozi hiyo mpya ya mipango miji. Bw. Musa alisema kuwa, “Programu ya Mipango Miji (Urban and Regional Planning) kwa ngazi ya Astashahada (NTA 4) na Stashahada (NTA 5) zitaanza rasmi mwaka wa masomo 2018/2019 mnamo mwezi wa kumi”. Bi. Kamihanda anasema kuwa wanao wakufunzi wa Mipango miji na anahimiza wale wenye sifa kupakua fomu za maombi katika tovuti ya chuo www.arimo.ac.tz. Pia amewahimiza wasichana kuchangamkia fursa hiyo.

Safu hii imebahatika kupakua fomu za maombi kutoka tovuti ya chuo. Miongoni mwa mambo muhimu katika fomu hiyo ni sifa za kujiunga na kozi ya hii ya mipango miji chuoni ARIMO. Kwa waombaji wa Astashahada (Basic Certificate in URP) - NTA Level 4 wanapaswa kuwa wamehitimu kidato cha nne na kufaulu masomo (4) au zaidi katika masomo ya Jiografia, Hisabati, Fizikia, Kemia, Bailojia, Kingereza, Biashara na Historia.

Kwa waombaji wa Stashahada (Diploma in URP) - NTA Level 5-6 lazima wawe wahitimu kidato cha sita na wenye alama “E” na “S” katika masomo mawili ya sayansi AU amemaliza astashahada ya Chuo cha Ardhi Morogoro au Chuo kingine chochote kinachotambuliwa na NACTE katika fani za Mipango Miji (Urban and Regional Planning), Utawala wa Ardhi (Land Management), Jiomatikia (Geomatics), Uandaaji Ramani (Cartography) AU astashahada inayoshabihiana na Uhandisi (Related Engineering Certificate).

Hivi ndivyo wanataaluma na mafundi mchundo wa chuo cha Ardhi Morogoro wanavyoadhimisha miaka arobaini ya uwepo wa chuo. Wanakuja kivingine.